Habari
BRELA YAUNGANA NA WATANZANIA KUADHIMISHA MEI MOSI 2026
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) leo, tarehe 01 Mei 2026, umeungana na wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi nchini kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi).
Maadhimisho ya kitaifa yamefanyika mkoani Njombe yakiongozwa na kaulimbiu isemayo: “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050.” Mgeni rasmi katika sherehe hizo alikuwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akihutubia wafanyakazi, Rais Dkt. Samia alisisitiza kuwa licha ya changamoto za kiuchumi zinazoikabili dunia, Serikali itaendelea kuhakikisha Watanzania wanakuwa na hali bora na salama ya maisha.
“Kama mnavyosikia duniani, kuna mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoathiri hasa nchi zinazoendelea. Hata hivyo, ni lazima tushirikiane kukabiliana na hali hii ili kulinda ustawi wa taifa letu,” amesema Rais Dkt. Samia.
Kwa upande wa Mkoa wa Dar es Salaam, maadhimisho hayo yamefanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja na kuhudhuriwa na wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali, ikiwemo BRELA. Mgeni rasmi katika ngazi ya mkoa alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, amewapongeza watumishi wa taasisi hiyo na kuwataka kuitumia siku hii muhimu kujikumbusha kuwa wao ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa malengo ya Serikali, hususan katika nyanja ya urasimishaji wa biashara.
“Kupitia siku hii, ni muhimu umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa weledi ili kusaidia Serikali kufikia malengo yake. Serikali pia itaendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji kazi,” amesema Bw. Nyaisa.
Katika hatua nyingine, Bw. Nyaisa amempongeza mfanyakazi hodari wa taasisi hiyo kwa mwaka 2025/2026, Bw. Malema Siwakwi, na kuhimiza kuwa hatua hiyo iwe chachu ya kuongeza bidii kazini na kuwa hamasa kwa watumishi wengine.
Ushiriki wa BRELA katika maadhimisho haya unaonesha dhamira yake katika kuunga mkono kaulimbiu ya mwaka huu. Kurahisisha na kuhimiza urasimishaji wa biashara kupitia usajili wa majina ya biashara na makampuni ni hatua muhimu katika kukuza uchumi endelevu na kufikia malengo ya Dira ya Taifa 2050.
