Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

ELIMU YA URASIMISHAJI BIASHARA YAWAFIKIA WANAFUNZI CHUO CHA WAISLAMU MOROGORO (MUM)


Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 18, Februari 2026, Afisa Usajili wa BRELA Bi. Maryglory Mmari alisema mkakati huo maalum wa kuyafikia makundi mbalimbali ya vijana, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali umelenga zaidi kuwajengea uwezo na kuwaongeza uelewa vijana juu ya masala ya urasimishaji biashara.

Bi. Mmari alitoa wito pia kwa wafanyabiashara hasa vijana kutumia elimu inayotolewa na Wakala akisema kuwa urasimishaji ni hatua muhimu inayomwezesha mjasiriamali kupata fursa mbalimbali ikiwemo mikopo kutoka taasisi za fedha, kuingia mikataba halali ya kibiashara, kulinda jina na kujenga uaminifu kwa wateja.

Kwa upande wake Mhadhiri Msaidizi wa Chuo hicho, Bw. Rashid Yusuph alisema ujio wao katika Ofisi za BRELA umekuwa na manufaa makubwa kwa wanafunzi wa masomo ya biashara kwani wamepata fursa ya kujifunza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa usajili wa Biashara na Leseni za Biashara

“Wanafunzi tunawafundisha masomo mbalimbali ikiwemo ya biashara, lakini kupitia mafunzo haya wamejifunza kwa wataalamu wa usajili na watoaji wa leseni za biashara moja kwa moja, tunaamini mafunzo haya yamewasaidia kupata uelewa mpana zaidi kuhusu masuala ya usajili na urasimishaji wa biashara,” alisema Bw. Rashid.

Kwa upande wao wanafunzi waliozungumza baada ya mafunzo hayo, Issa Mohamed Issa na Hawa Kismart Abdi walisema elimu waliyoipata ni kubwa zaidi ukilinganisha na matarajio yao ya awali na kwamba mafunzo waliyopata yamewapa mwanga juu ya taratibu sahihi za kuanzisha na kuendesha biashara.

“Tumejifunza namna ya kulinda mtaji wetu, kusajili na kulinda nembo (logo) ya biashara, pamoja na kufanya biashara kwa kufuata sheria ili kupata faida halali na endelevu,” alisema Issa.