Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Tunaipa Uhai wa Kisheria Biashara yako

Habari

TAASISI ZA SERIKALI ZATAKIWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA UKUAJI WA VIWANDA


TAASISI ZA SERIKALI ZATAKIWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KWA UKUAJI WA VIWANDA

 

Watendaji wa taasisi za Serikali wametakiwa kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia uanzishaji wa  viwanda nchini.

 

Wito huo umetolewa na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya  Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaban, tarehe 4 Desemba, 2022 wakati  akifungua rasmi Maonesho ya Saba  ya Tanzania katika Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

 

Mhe. Shabaan amesema sekta ya viwanda ni nyezo muhimu ya kufanikisha malengo ya dira ya maendeleo ifikapo 2025 ya kufikia uchumi wa kati ya juu, hivyo mazingira wezeshi kwa maendeleo ya uwekezaji wa viwanda yatasaidia kufikia malengo hayo.

 

"Taasisi  za Serikali zinapaswa kutekeleza ipasavyo mpango wa kuboresha mazingira ya biashara ili kuwezesha ukuaji wa sekta ya viwanda nchini", amefafanua Mhe.

Shaaban.

 

Awali Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Mhe. Ally Gugu akimkaribisha  Waziri Shaaban wa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Ashatu Kijaji amewataka waandaaji na washiriki wa maonesho hayo kuhakikisha kuwa wanatekeleza kwa vitendo kwa kununua bidhaa za Tanzania ili kujenga Tanzania kama kauli mbiu ya maonesho hayo inavyoeleza.

 

Amesema fursa hii itumike pia kujitangaza sambamba na uzalishaji wa bidhaa bora zinazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

  

Maonesho  hayo ya bidhaa za Viwanda vya Tanzania yenye kauli mbiu ya "Nunua bidhaa ya Tanzania Jenga Tanzania #Nunua cha Kwetu" yameanza terehe 03 Desemba, 2022 na yatahitimishwa tarehe 09 Desemba, 2022 huku BRELA ikishiriki kikamilifu kutoa huduma za urasimishaji wa biashara.