Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni

Lango la Mafanikio ya Biashara

Habari

URASIMISHAJI WA BIASHARA NI UFUNGUO WA FURSA ZA KIUCHUMI KWA VIJANA


Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imewahimiza vijana kurasimisha biashara na kulinda Miliki Bunifu zao ili kupata fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali pamoja na kuimarisha ushindani wa biashara zao katika soko.

Wito huo umetolewa leo, Novemba 27, 2026, wakati wa mafunzo maalumu ya urasimishaji wa biashara kwa wanafunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) yaliyolenga kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kusajili majina ya biashara kampuni pamoja na ulinzi wa Miliki Ubunifu.

Akizungumza katika mafunzo Afisa Sheria wa BRELA, Bi. Neema Nyadzi alieleza kuwa usajili wa jina la biashara ni hatua muhimu katika kuitambulisha biashara sokoni, kujenga uaminifu kwa wateja na kuiwezesha biashara kutambulika kisheria.

Aidha aliwahimiza vijana kutokuchukulia usajili wa biashara kama utaratibu wa kisheria pekee, bali kama hatua muhimu inayofungua milango ya fursa ikiwemo kushiriki katika zabuni na programu za Serikali zinazolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.

“Vijana wanapaswa kutambua kuwa kufanya biashara hakumaanishi kuwa na duka au eneo la kufanyia biashara bali wanaweza kutumia ujuzi, maarifa na ubunifu wako kuanzisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuzirasimisha ili ziweze kukua na kushindana katika soko.” 

Kwa upande wake, Afisa Sheria kutoka Kurugenzi ya Miliki Ubunifu ya BRELA, Bw. George Msaki alitoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda bunifu zinazozalishwa na wanafunzi huku akisisitiza umuhimu wanachukua hatua za kisheria kulinda bunifu zao kabla ya kuzitangaza au kuzibainisha kwa umma.

“Ulinzi wa bunifu ni sehemu muhimu ya kulinda matokeo ya ubunifu na kuhakikisha wabunifu wanatambuliwa na kuwa na fursa ya kunufaika na kazi zao kabla ya watu wengine hawajanufaika nao” alisema Bw. Msaki

Nao wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo walisema elimu waliyoipata itakuwa na manufaa makubwa baada ya kuhitimu masomo yao hususan katika kuanzisha Biashara zao na kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Vilevile, walisema kupitia elimu hiyo wamepata uelewa utakaowawezesha kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha vijana wengine kuhusu umuhimu wa kurasimisha biashara na kulinda bunifu zao ili wawez nie kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi

BRELA inaendelea kuhamasisha wafanyabiashara hasa kundi la vijana nchini kurasimisha biashara zao ili waweze kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.