Habari
VIJANA JIJINI MBEYA WAKUMBUSHWA KUTUMIA HUDUMA ZA BRELA KUKUZA BIASHARA ZAO
Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika kutekeleza majukumu yake, tarehe 25 Mei 2026 ilitoa wito kwa vijana wa jiji la Mbeya kuchagamkia fursa ya kurasimisha na kusajili biashara ili kuongeza thamani, kupata fursa za mikopo na kukuza uchumi wao.
Wito huo umetolewa na Afisa Leseni Mwandamizi kutoka BRELA Bw. Koyan Aboubakar alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na Radio Bomba FM jijini humo kuhusu mkakati wa Wakala katika kuwasaidia vijana kukuza biashara zao.
"Tunajua vijana wengi wa Mbeya na mikoa ya jirani ni wabunifu na wanajihusisha na ujasiriamali, BRELA tunawasihi vijana wasibaki nje ya mfumo rasmi kwani wakirasimisha biashara, wanajifungulia milango ya kupata mikopo, wanajenga uaminifu kwa wateja na wanapata pia fursa ya kushiriki zabuni mbalimbali za serikali na sekta binafisi” alisema Bw. Koyan
Aidha Bw. Koyan pia alisisitiza kuwa kwa sasa BRELA inatumia mfumo mpya wa usajili unaojulikana kama BOS (BRELA Online Services) ambao umeboreshwa na unapatikana kwa njia ya mtandao, jambo linalofanya huduma hizo kuwa rahisi, za haraka na zenye gharama nafuu kwa wadau wake wote hasa vijana.
Akijibu swali kuhusu faida za vijana kurasimisha biashara zao, Bw. Koyan alisema kama ilivyo kauli mbiu ya Wakala kuwa “BRELA Lango la Mafanikio ya Biashara” vijana wanaposajili Majina ya Biashara, Kampuni na kumiliki Leseni za Biashara, kulinda Alama zao za Biashara na Huduma wanapata faida kubwa ya ulinzi wa kisheria.
BRELA inashiriki maonyesho ya Mbeya City Expo 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Uhindini, kwa kutoa huduma za papo kwa papo ikiwemo elimu ya urasimishaji biashara kwa wananchi na wafanyabiashara wanaotembelea banda lake katika hivyo.
